Afadhali kwenda kwenye nyumba ya msiba kuliko kwenda kwenye nyumba ya karamu, kwa kuwa kifo ni hatima ya kila mwanadamu, imewapasa walio hai kuliweka hili mioyoni mwao.
Moyo wa wenye hekima uko katika nyumba ya msiba, lakini moyo wa wapumbavu uko katika nyumba ya anasa.
Kama ilivyo kuvunjika kwa miiba chini ya sufuria, ndivyo kilivyo kicheko cha wapumbavu. Hili nalo pia ni ubatili.
Usiseme, “Kwa nini siku za kale zilikuwa bora kuliko siku hizi?” Kwa maana si hekima kuuliza maswali kama hayo.
Hekima ni ulinzi kama fedha ilivyo ulinzi, lakini faida ya maarifa ni hii: kwamba hekima huhifadhi maisha ya aliye nayo.
Nyakati zikiwa nzuri, ufurahi, lakini nyakati zikiwa mbaya, tafakari: Mungu amefanya hiyo moja, naam, sanjari na hiyo nyingine. Kwa hiyo, mwanadamu hawezi kugundua kitu chochote kuhusu maisha yake ya baadaye.
Katika maisha haya yangu ya ubatili nimeshaona haya mawili: mtu mwadilifu akiangamia katika uadilifu wake, naye mtu mwovu akiishi maisha marefu katika uovu wake.
Ni vyema kushika hilo moja na wala usiache hilo jingine likupite. Mtu amchaye Mungu ataepuka huko kupita kiasi.
Yote haya niliyajaribu kwa hekima, nikasema, “Nimeamua kuwa na hekima”: lakini hii ilikuwa nje ya uwezo wangu.
Nikageuza fikira zangu ili kuelewa, kuchunguza na kuitafuta hekima na kusudi la mambo, na ili kuelewa ujinga wa uovu, na wazimu wa upumbavu.
Nimeona jambo lililo chungu kuliko mauti, mwanamke ambaye ni mtego, ambaye moyo wake ni wavu wa kutegea na mikono yake ni minyororo. Mtu ampendezaye Mungu atamkwepa, bali mwenye dhambi atanaswa naye.
Mhubiri anasema, “Tazama, hili ndilo nililogundua: “Nimegundua kitu kimoja baada ya kingine nilipokuwa katika kusudi la mambo:
ningali natafiti lakini sipati: nilimpata mwanaume mmoja mnyofu miongoni mwa elfu, lakini hakuna mwanamke mmoja mnyofu miongoni mwao.