Mungu humpa mwanadamu utajiri, mali na heshima, hivyo hakukosa chochote moyo wake unachokitamani. Lakini Mungu hamwezeshi kuvifurahia, badala yake mgeni ndiye anayevifurahia. Hili ni ubatili, ni ubaya unaosikitisha.
Mtu anaweza kuwa na watoto mia moja naye akaishi miaka mingi, lakini haidhuru kuwa ataishi muda mrefu kiasi gani, kama hawezi kufurahia mafanikio yake na kwamba hapati mazishi ya heshima, ninasema afadhali mtoto aliyezaliwa akiwa amekufa kuliko yeye.
Hata kama huyo mtu ataishi miaka elfu mara mbili na zaidi, lakini akashindwa kufurahia mafanikio yake, je, wote hawaendi sehemu moja?
Mtu mwenye hekima ana faida gani zaidi ya mpumbavu? Mtu maskini anapata faida gani kwa kujua jinsi ya kujistahi mbele ya watu wengine?
Ni bora kile ambacho jicho linakiona kuliko hamu isiyotoshelezwa. Hili nalo ni ubatili, ni kukimbiza upepo.
Lolote lililopo limekwisha kupewa jina, naye mwanadamu alivyo ameshajulikana; hakuna mtu awezaye kushindana na mwenye nguvu kuliko yeye.