Ni nani aliye kama mtu mwenye hekima? Ni nani ajuaye maelezo ya mambo? Hekima hungʼarisha uso wa mtu na kubadili ugumu wa uso wake.
Usiharakishe kuondoka mbele ya mfalme. Usiendelee kutenda lililo baya, kwa maana mfalme atafanya lolote apendalo.
Kwa kuwa neno la mfalme ndilo lenye mamlaka ya mwisho, nani awezaye kumwambia, “Je, wewe unafanya nini?”
Kwa maana kuna wakati muafaka na utaratibu wa kila jambo, ingawa huzuni ya mwanadamu huwa nzito juu yake.
Hakuna mwanadamu awezaye kushikilia roho yake asife, wala hakuna mwenye uwezo juu ya siku ya kufa kwake. Kama vile hakuna yeyote arudishwaye nyuma wakati wa vita, kadhalika uovu hautawaweka huru wale wautendao.
Yote haya niliyaona, nilipokuwa natafakari kila kitu kinachotendeka chini ya jua. Kuna wakati ambapo mtu hujifanya bwana juu ya wengine kwa madhara yake mwenyewe.
Ndipo pia, nikaona waovu wakizikwa, wale ambao walizoea kuingia na kutoka mahali patakatifu na kupewa sifa katika mji ambapo walikuwa wamefanya haya. Hili nalo ni ubatili.
Ingawa mtu mwovu hufanya maovu mia moja na akaendelea kuishi maisha marefu, najua kwamba itakuwa bora zaidi kwa watu wanaomwogopa Mungu, wamchao Mungu.
Kuna kitu kingine ambacho ni ubatili kinachotokea duniani: Watu waadilifu kupata yale yanayowastahili waovu, nao waovu kupata yale yanayowastahili waadilifu. Hili nalo pia, nasema ni ubatili.
Kwa hiyo mimi ninasifu kufurahia maisha, kwa sababu hakuna kitu bora zaidi kwa mwanadamu chini ya jua kuliko kula, kunywa na kufurahi. Kisha furaha itafuatana naye kazini mwake siku zote za maisha yake ambazo amepewa na Mungu chini ya jua.
Nilipotafakari akilini mwangu ili nijue hekima na kuangalia kazi ya mwanadamu duniani, jinsi ambavyo macho yake hayapati usingizi mchana wala usiku,