Tazama sasa, Bwana, Bwana Mwenye Nguvu Zote, yu karibu kuwaondolea Yerusalemu na Yuda upatikanaji wa mahitaji na misaada, upatikanaji wote wa chakula na tegemeo lote la maji,
Watu wataoneana wao kwa wao: mtu dhidi ya mtu, na jirani dhidi ya jirani yake. Kijana atainuka dhidi ya mzee, mtu mnyonge dhidi ya mtu mwenye heshima.
Mtu atamkamata mmoja wa ndugu zake katika nyumba ya baba yake na kusema, “Unalo joho, sasa uwe kiongozi wetu, tawala lundo hili la magofu!”
Lakini siku hiyo atapiga kelele akisema, “Sina uponyaji. Sina chakula wala mavazi katika nyumba yangu, msinifanye niwe kiongozi wa watu.”
Yerusalemu inapepesuka, Yuda inaanguka; maneno yao na matendo yao ni kinyume na Bwana, wakiudharau uwepo wake uliotukuka.
Nyuso zao zinavyoonekana zinashuhudia dhidi yao, hujivunia dhambi yao kama Sodoma, wala hawaifichi. Ole wao! Wamejiletea maafa juu yao wenyewe.
Vijana wanawatesa watu wangu, wanawake wanawatawala. Enyi watu wangu, viongozi wenu wanawapotosha, wanawapoteza njia.
Bwana anaingia katika hukumu dhidi ya wazee na viongozi wa watu wake: “Ninyi ndio mlioharibu shamba langu la mizabibu, mali zilizonyangʼanywa maskini zimo nyumbani mwenu.
Mnamaanisha nini kuwaponda watu wangu na kuzisaga nyuso za maskini?” asema Bwana, Bwana Mwenye Nguvu Zote.
Bwana asema, “Wanawake wa Sayuni wana kiburi, wanatembea na shingo ndefu, wakikonyeza kwa macho yao, wanatembea kwa hatua za madaha, wakiwa na mapambo ya njuga kwenye vifundo vya miguu yao.
Kwa hiyo Bwana ataleta majipu kwenye vichwa vya wanawake wa Sayuni; Bwana atazifanya ngozi za vichwa vyao kuwa vipara.”
Katika siku ile Bwana atawanyangʼanya uzuri wao: bangili, tepe za kichwani, mikufu yenye alama za mwezi mwandamo,
Badala ya harufu ya manukato kutakuwa na uvundo; badala ya mishipi, ni kamba; badala ya nywele zilizotengenezwa vizuri, ni upara; badala ya mavazi mazuri, ni nguo za magunia; badala ya uzuri, ni alama ya aibu kwa chuma cha moto.