Katika siku za mwisho mlima wa Hekalu la Bwana utaimarishwa kama mlima mkuu miongoni mwa milima yote, utainuliwa juu ya vilima, na mataifa yote yatamiminika huko.
Mataifa mengi yatakuja na kusema, “Njooni, twendeni mlimani mwa Bwana, kwenye nyumba ya Mungu wa Yakobo. Atatufundisha njia zake, ili tuweze kuenenda katika mapito yake.” Sheria itatoka Sayuni, neno la Bwana litatoka Yerusalemu.
Atahukumu kati ya mataifa na ataamua migogoro ya mataifa mengi. Watafua panga zao ziwe majembe, na mikuki yao kuwa miundu ya kukata matawi. Taifa halitainua upanga dhidi ya taifa jingine, wala hawatajifunza vita tena.
Umewatelekeza watu wako, nyumba ya Yakobo. Wamejaa ushirikina utokao Mashariki, wanapiga ramli kama Wafilisti na wanashikana mikono na wapagani.
Nchi yao imejaa fedha na dhahabu, hakuna mwisho wa hazina zao. Nchi yao imejaa farasi, hakuna mwisho wa magari yao.
Macho ya mtu mwenye majivuno yatanyenyekezwa na kiburi cha wanadamu kitashushwa, Bwana peke yake ndiye atakayetukuzwa siku hiyo.
Bwana Mwenye Nguvu Zote anayo siku aliyoiweka akiba kwa wote wenye kujivuna na wenye kiburi, kwa wote wanaojikweza (nao watanyenyekezwa),
Majivuno ya mwanadamu yatashushwa, na kiburi cha wanadamu kitanyenyekezwa, Bwana peke yake ndiye atatukuzwa siku hiyo,
Watu watakimbilia kwenye mapango ndani ya miamba, na kwenye mahandaki ardhini kutokana na utisho wa Bwana na utukufu wa enzi yake, ainukapo kuitikisa dunia.
Siku ile, watu watawatupia panya na popo sanamu zao za fedha na za dhahabu, walizozitengeneza ili waziabudu.
Watakimbilia kwenye mapango miambani na kwenye nyufa za miamba kutokana na utisho wa Bwana na utukufu wa enzi yake, ainukapo kuitikisa dunia.