Nitaimba juu ya upendo mkuu wa Bwana milele; kwa kinywa changu nitajulisha uaminifu wako ujulikane kwa vizazi vyote.
Kwa kuwa ni nani katika mbingu anayeweza kulinganishwa na Bwana? Ni nani miongoni mwa viumbe vya mbinguni aliye kama Bwana?
Ee Bwana Mwenye Nguvu Zote, ni nani aliye kama wewe? Ee Bwana, wewe ni mwenye nguvu, na uaminifu wako unakuzunguka.
Wewe ulimponda Rahabu kama mmojawapo wa waliochinjwa; kwa mkono wako wenye nguvu, uliwatawanya adui zako.
Heri ni wale ambao wamejifunza kukusifu kwa shangwe, wanaotembea katika mwanga wa uwepo wako, Ee Bwana.
Ulizungumza wakati fulani katika maono, kwa watu wako waaminifu, ukasema: “Nimeweka nguvu kwa shujaa, nimemwinua kijana miongoni mwa watu.
Bwana kumbuka jinsi mtumishi wako amesimangwa, jinsi ninavyovumilia moyoni mwangu dhihaka za mataifa yote,
dhihaka ambazo kwazo adui zako wamenisimanga, Ee Bwana, ambazo kwazo wamesimanga kila hatua ya mpakwa mafuta wako.