Akanipandisha kutoka shimo la uharibifu, kutoka matope na utelezi; akaiweka miguu yangu juu ya mwamba na kunipa mahali imara pa kusimama.
Akaweka wimbo mpya kinywani mwangu, wimbo wa sifa kwa Mungu wetu. Wengi wataona na kuogopa na kuweka tumaini lao kwa Bwana.
Heri mtu yule amfanyaye Bwana kuwa tumaini lake, asiyewategemea wenye kiburi, wale wenye kugeukia miungu ya uongo.
Ee Bwana Mungu wangu, umefanya mambo mengi ya ajabu. Mambo uliyopanga kwa ajili yetu hakuna awezaye kukuhesabia; kama ningesema na kuyaelezea, yangekuwa mengi mno kuyaelezea.
Dhabihu na sadaka hukuvitaka, lakini umefungua masikio yangu; sadaka za kuteketezwa na sadaka za dhambi hukuzihitaji.
Sikuficha haki yako moyoni mwangu; ninasema juu ya uaminifu wako na wokovu wako. Sikuficha upendo wako na kweli yako mbele ya kusanyiko kubwa.
Kwa maana taabu zisizo na hesabu zimenizunguka, dhambi zangu zimenikamata, hata nisiweze kuona. Zimekuwa nyingi kuliko nywele za kichwa changu, nao moyo unazimia ndani yangu.
Wote wanaotafuta kuuondoa uhai wangu, waaibishwe na kufadhaishwa; wote wanaotamani kuangamizwa kwangu, warudishwe nyuma kwa aibu.
Lakini wote wakutafutao washangilie na kukufurahia, wale wapendao wokovu wako siku zote waseme, “Bwana atukuzwe!”