Bwana ni mwamba wangu, ngome yangu na mwokozi wangu, Mungu wangu ni mwamba, ambaye kwake ninakimbilia. Yeye ni ngao yangu na pembe ya wokovu wangu, ngome yangu.
Katika shida yangu nalimwita Bwana, nilimlilia Mungu wangu anisaidie. Kutoka hekaluni mwake alisikia sauti yangu, kilio changu kikafika mbele zake, masikioni mwake.
Dunia ilitetemeka na kutikisika, misingi ya milima ikatikisika, vilitetemeka kwa sababu alikuwa amekasirika.
Moshi ukapanda kutoka puani mwake, moto uteketezao ukatoka kinywani mwake, makaa ya moto yawakayo yakatoka ndani mwake.
Alifanya giza kuwa kitu chake cha kujifunika, hema lake kumzunguka, mawingu meusi ya mvua ya angani.
Mabonde ya bahari yalifunuliwa, na misingi ya dunia ikawa wazi kwa kukaripia kwako, Ee Bwana, kwa uvumi wa pumzi kutoka puani mwako.
Aliniokoa kutoka adui wangu mwenye nguvu nyingi, kutoka adui zangu waliokuwa na nguvu nyingi kuliko mimi.
Kwa yeye aliye mwaminifu, unajionyesha kuwa mwaminifu, kwa asiye na hatia, unajionyesha kutokuwa na hatia.
Kuhusu Mungu, njia yake ni kamilifu, neno la Bwana halina dosari. Yeye ni ngao kwa wote wanaokimbilia kwake.
Umeniokoa kutokana na mashambulizi ya watu; umenifanya kuwa kiongozi wa mataifa, watu ambao sikuwajua wananitumikia.