Mwache mwingine akusifu, wala si kinywa chako mwenyewe; mtu mwingine afanye hivyo na si midomo yako mwenyewe.
Yeye aliyeshiba huchukia kabisa asali, bali kwa mwenye njaa hata kile kilicho kichungu kwake ni kitamu.
Kama ndege atangatangavyo mbali na kiota chake, ndivyo alivyo mtu atangatangaye mbali na nyumbani mwake.
Manukato na uvumba huleta furaha moyoni, nao uzuri wa rafiki huchipuka kutoka kwenye ushauri wake wa uaminifu.
Usimwache rafiki yako wala rafiki wa baba yako, tena usiende nyumbani mwa ndugu yako wakati umepatwa na maafa. Bora jirani wa karibu kuliko ndugu aliye mbali.
Mwanangu, uwe na hekima, nawe ulete furaha moyoni mwangu, ndipo nitakapoweza kumjibu yeyote anitendaye kwa dharau.
Chukua vazi la yule awekaye dhamana kwa ajili ya mgeni; lishikilie iwe dhamana kama anafanya hivyo kwa ajili ya mwanamke mpotovu.