“Waisraeli watapiga kambi zao kuzunguka Hema la Kukutania kwa umbali fulani kutoka kwenye hema, kila mwanaume chini ya alama yake pamoja na bendera ya jamaa yake.”
Kwa upande wa mashariki kuelekea mawio ya jua, kambi ya makundi ya Yuda watapiga kambi chini ya alama yao. Kiongozi wa watu wa Yuda ni Nashoni mwana wa Aminadabu.
Kabila la Isakari watapiga kambi karibu na Yuda. Kiongozi wa watu wa Isakari ni Nethaneli mwana wa Suari.
Wanaume wote walio katika kambi ya Yuda, kufuatana na makundi yao, ni 186,400. Wao watatangulia kuondoka.
Kwa upande wa kusini kutakuwa kambi ya makundi ya Reubeni chini ya alama yao. Kiongozi wa watu wa Reubeni ni Elisuri mwana wa Shedeuri.
Kabila la Simeoni watapiga kambi karibu na Reubeni. Kiongozi wa watu wa Simeoni ni Shelumieli mwana wa Surishadai.
Wanaume wote walio katika kambi ya Reubeni, kufuatana na makundi yao, ni 151,450. Nao watakuwa nafasi ya pili kuondoka.
Kisha Hema la Kukutania na kambi ya Walawi vitakuwa katikati ya kambi zote. Wao watasafiri kwa utaratibu ule ule kama walivyopiga kambi, kila mmoja mahali pake mwenyewe chini ya alama yake.
Upande wa magharibi kutakuwepo na kambi ya makundi ya Efraimu chini ya alama yao. Kiongozi wa watu wa Efraimu ni Elishama mwana wa Amihudi.
Kabila la Manase litafuata baada ya Efraimu. Kiongozi wa watu wa Manase ni Gamalieli mwana wa Pedasuri.
Kabila la Benyamini litafuata baada ya Manase. Kiongozi wa watu wa Benyamini ni Abidani mwana wa Gideoni.
Wanaume wote walio katika kambi ya Efraimu kufuatana na makundi yao ni 108,100. Nao watakuwa nafasi ya tatu kuondoka.
Upande wa kaskazini kutakuwa na makundi ya kambi ya Dani, chini ya alama yao. Kiongozi wa watu wa Dani ni Ahiezeri mwana wa Amishadai.
Kabila la Asheri watapiga kambi karibu na Dani. Kiongozi wa watu wa Asheri ni Pagieli mwana wa Okrani.
Wanaume wote walio katika kambi ya Dani ni 157,600. Wao watakuwa wa mwisho kuondoka chini ya alama yao.
Hawa ndio Waisraeli, wakiwa wamehesabiwa kufuatana na jamaa zao. Wote walio kambini kwa makundi yao ni watu 603,550.