Bwana ni mwenye wivu na Mungu mlipiza kisasi; Bwana hulipiza kisasi na amejaa ghadhabu. Bwana hulipiza kisasi juu ya watesi wake, naye anadumisha ghadhabu yake dhidi ya adui zake.
Bwana si mwepesi wa hasira naye ni mwenye nguvu, Bwana hataacha kuadhibu wenye hatia. Njia yake ipo katika kisulisuli na tufani, na mawingu ni vumbi la miguu yake.
Anakemea bahari na kuikausha, anafanya mito yote kukauka. Bashani na Karmeli zinanyauka na maua ya Lebanoni hukauka.
Milima hutikisika mbele yake na vilima huyeyuka. Nchi hutetemeka mbele yake, dunia na wote waishio ndani yake.
Ni nani awezaye kuzuia hasira yake yenye uchungu? Nani awezaye kuvumilia hasira yake kali? Ghadhabu yake imemiminwa kama moto, na miamba inapasuka mbele zake.
Ee Ninawi, kutoka kwako amejitokeza mmoja, ambaye anapanga shauri baya dhidi ya Bwana na kushauri uovu.
Hili ndilo asemalo Bwana: “Ingawa wana muungano nao ni wengi sana, watakatiliwa mbali na kuangamia. Ingawa nimekutesa wewe, ee Yuda, sitakutesa tena.
Hii ndiyo amri Bwana aliyoitoa kukuhusu wewe, Ninawi: “Hutakuwa na wazao watakaoendeleza jina lako. Nitaharibu sanamu za kuchonga na sanamu za kuyeyusha ambazo zipo katika hekalu la miungu yenu. Nitaandaa kaburi lako, kwa maana wewe ni mwovu kabisa.”