Baada ya haya Yesu alikwenda, akawa anazunguka katika miji na vijiji akihubiri habari njema za Ufalme wa Mungu. Wale wanafunzi wake kumi na wawili walikuwa pamoja naye,
pia baadhi ya wanawake waliokuwa wametolewa pepo wachafu na kuponywa magonjwa. Miongoni mwao alikuwepo Maria Magdalene, aliyetolewa pepo wachafu saba;
Yoana mkewe Kuza, msimamizi wa nyumba ya watu wa nyumbani mwa Herode; Susana; na wengine wengi waliokuwa wakimhudumia kwa mali zao.
“Mpanzi alitoka kwenda kupanda mbegu zake. Alipokuwa akitawanya mbegu, nyingine zilianguka kando ya njia; zikakanyagwa, nao ndege wa angani wakazila.
Nazo mbegu nyingine zilianguka kwenye miiba, nayo ile miiba ikakua pamoja nazo, na kuisonga hiyo mimea.
Mbegu nyingine zilianguka kwenye udongo mzuri. Zikaota na kuzaa mara mia moja zaidi ya mbegu alizopanda.” Baada ya kusema haya, Yesu akapaza sauti, akasema, “Mwenye masikio ya kusikia, na asikie.”
Naye akasema, “Ninyi mmepewa kufahamu siri za Ufalme wa Mungu, lakini kwa wengine nazungumza kwa mifano, ili, “ ‘ingawa wanatazama, wasione; ingawa wanasikiliza, wasielewe.’
Zile zilizoanguka kando ya njia ni wale ambao husikia neno, naye ibilisi anakuja na kuliondoa neno kutoka mioyoni mwao, ili wasije wakaamini na kuokoka.
Zile mbegu zilizoanguka kwenye mwamba ni wale ambao hulipokea neno kwa furaha wanapolisikia, lakini hawana mizizi. Wanaamini kwa muda mfupi, lakini wakati wa kujaribiwa huiacha imani.
Zile mbegu zilizoanguka kwenye miiba ni mfano wa wale wanaosikia, lakini wanapoendelea husongwa na masumbufu ya maisha haya, utajiri na anasa, nao hawakui.
Lakini zile mbegu zilizoanguka kwenye udongo mzuri ni mfano wa wale ambao hulisikia neno la Mungu na kulishika kwa moyo mnyofu wa utiifu, nao kwa kuvumilia kwingi huzaa matunda.
“Hakuna mtu awashaye taa na kuificha ndani ya gudulia au kuiweka mvunguni mwa kitanda. Badala yake, huiweka juu ya kinara, ili wale waingiao ndani waone mwanga.
Kwa maana hakuna jambo lolote lililofichika ambalo halitafichuliwa, wala lolote lililositirika ambalo halitajulikana na kuwekwa wazi.
Kwa hiyo, kuweni waangalifu mnavyosikia. Kwa maana yeyote aliye na kitu atapewa zaidi. Lakini yule asiye na kitu, hata kile anachodhani anacho atanyangʼanywa.”
Wakati mmoja mama yake Yesu na ndugu zake walikuja kumwona, lakini hawakuweza kumfikia kwa sababu ya msongamano wa watu.
Siku moja Yesu alipanda ndani ya mashua pamoja na wanafunzi wake, akawaambia, “Tuvukeni twende mpaka ngʼambo ya ziwa.” Nao wakaondoka.
Hivyo walipokuwa wakienda, akalala usingizi. Dhoruba kali ikatokea mle ziwani, hata mashua ikawa inajaa maji, nao walikuwa katika hatari kubwa.
Wanafunzi wake wakamwendea na kumwamsha, wakisema, “Bwana, Bwana, tunaangamia!” Yeye akaamka, akaukemea ule upepo na yale mawimbi; dhoruba ikakoma, nako kukawa shwari.
Akawauliza wanafunzi wake, “Imani yenu iko wapi?” Kwa woga na mshangao wakaulizana, “Huyu ni nani, ambaye anaamuru hata upepo na maji, navyo vikamtii?”
Yesu aliposhuka kutoka mashua na kukanyaga ufuoni, alikutana na mtu mmoja wa mji ule aliyekuwa amepagawa na pepo mchafu, naye kwa muda mrefu alikuwa havai nguo wala kuishi nyumbani, bali aliishi makaburini.
Alipomwona Yesu, alipiga kelele, akajitupa chini mbele yake na kusema kwa sauti kuu, “Una nini nami, Yesu, Mwana wa Mungu Aliye Juu Sana? Nakuomba, usinitese!”
Wakati huo Yesu alikuwa amemwamuru yule pepo mchafu amtoke huyo mtu. Mara nyingi huyo pepo mchafu alimpagaa, na hata alipofungwa kwa minyororo mikono na miguu na kuwekwa chini ya ulinzi, alikata hiyo minyororo na kupelekwa na huyo pepo mchafu kwenda nyikani.
Yesu akamuuliza, “Jina lako ni nani?” Akamjibu, “Legioni,” kwa kuwa alikuwa ameingiwa na pepo wachafu wengi mno.
Palikuwa na kundi kubwa la nguruwe hapo likilisha kando ya kilima. Wale pepo wachafu wakamsihi Yesu awaruhusu wawaingie hao nguruwe, naye akawaruhusu.
Wale pepo wachafu walipomtoka yule mtu, wakawaingia wale nguruwe, nalo kundi lote likateremkia gengeni kwa kasi, likatumbukia ziwani na kuzama.
Wale watu waliokuwa wakichunga lile kundi la nguruwe walipoona yaliyotukia, wakakimbia, wakaeneza habari hizi mjini na mashambani.
Nao watu wakatoka kwenda kujionea wenyewe yaliyotukia. Walipofika hapo alipokuwa Yesu, wakamkuta yule mtu aliyetokwa na pepo wachafu amekaa karibu na Yesu, akiwa amevaa nguo na mwenye akili timamu! Wakaogopa.
Wale walioyaona mambo hayo wakawaeleza watu wengine jinsi yule mtu aliyekuwa amepagawa na pepo wachafu alivyoponywa.
Ndipo watu wote wa nchi ile ya Wagerasi wakamwomba Yesu aondoke kwao, kwa sababu walikuwa wamejawa na hofu. Basi akaingia katika mashua, akaondoka zake.
“Rudi nyumbani ukawaeleze mambo makuu Mungu aliyokutendea.” Kwa hiyo yule mtu akaenda, akatangaza katika mji wote mambo makuu ambayo Yesu alimtendea.
Kisha mtu mmoja, jina lake Yairo, aliyekuwa kiongozi wa sinagogi, akaja na kuanguka miguuni mwa Yesu, akimwomba afike nyumbani kwake,
kwa kuwa binti yake wa pekee, mwenye umri wa miaka kumi na miwili, alikuwa anakufa. Yesu alipokuwa akienda, umati wa watu ukamsonga sana.
Katika umati huo palikuwa na mwanamke mmoja aliyekuwa na tatizo la kutokwa damu kwa muda wa miaka kumi na miwili. Tena alikuwa amegharimia yote aliyokuwa nayo kwa ajili ya matibabu, wala hakuna yeyote aliyeweza kumponya.
Huyo mwanamke akaja kwa nyuma ya Yesu na kugusa upindo wa vazi lake. Mara kutokwa damu kwake kukakoma.
Yesu akauliza, “Ni nani aliyenigusa?” Watu wote walipokana, Petro akasema, “Bwana, huu umati wa watu unakusonga na kukusukuma kila upande.”
Yule mwanamke alipofahamu ya kuwa hawezi kuendelea kujificha, alikuja akitetemeka, akaanguka miguuni mwa Yesu. Akaeleza mbele ya watu wote kwa nini alimgusa na jinsi alivyoponywa mara.
Yesu alipokuwa bado anasema, akaja mtumishi kutoka nyumbani kwa Yairo, yule kiongozi wa sinagogi, kumwambia, “Binti yako amekwisha kufa. Usiendelee kumsumbua Mwalimu.”
Walipofika nyumbani kwa Yairo, hakumruhusu mtu yeyote aingie ndani naye isipokuwa Petro, Yakobo na Yohana, pamoja na baba na mama wa yule binti.
Wakati ule ule watu wote walikuwa wakilia na kuomboleza kwa ajili ya huyo binti. Yesu akawaambia, “Acheni kulia. Huyu binti hajafa, ila amelala.”