Sikilizeni hili, enyi wazee; sikilizeni, ninyi nyote mnaoishi katika nchi. Je, jambo kama hili lilishawahi kutokea katika siku zenu au katika siku za babu zenu?
Waelezeni watoto wenu, na watoto wenu wawaambie watoto wao, na watoto wao kwa kizazi kitakachofuata.
Kilichosazwa na kundi la tunutu nzige wakubwa wamekula, kilichosazwa na nzige wakubwa parare wamekula, kilichosazwa na parare madumadu wamekula.
Amkeni, enyi walevi, mlie! Pigeni yowe enyi wanywaji wote wa mvinyo, pigeni yowe kwa sababu ya mvinyo mpya, kwa kuwa mmenyangʼanywa kutoka midomoni mwenu.
Taifa limevamia nchi yangu, lenye nguvu tena lisilo na idadi; lina meno ya simba, magego ya simba jike.
Limeharibu mizabibu yangu na kuangamiza mitini yangu. Limebambua magome yake na kuyatupilia mbali, likayaacha matawi yake yakiwa meupe.
Sadaka za nafaka na sadaka za kinywaji zimekatiliwa mbali kutoka nyumba ya Bwana. Makuhani wanaomboleza, wale wanaohudumu mbele za Bwana.
Kateni tamaa, enyi wakulima, lieni, enyi mlimao mizabibu; huzunikeni kwa ajili ya ngano na shayiri, kwa sababu mavuno ya shambani yameharibiwa.
Mzabibu umekauka na mtini umenyauka; mkomamanga, mtende na mtofaa, miti yote shambani, imekauka. Hakika furaha yote ya mwanadamu imeondoka.
Vaeni nguo ya gunia, enyi makuhani, muomboleze; pigeni yowe, enyi mnaohudumu madhabahuni. Njooni, vaeni nguo ya gunia usiku kucha, enyi mnaohudumu mbele za Mungu wangu; kwa kuwa sadaka za nafaka na sadaka za kinywaji zimezuiliwa kufika katika nyumba ya Mungu wenu.
Tangazeni saumu takatifu; liiteni kusanyiko takatifu. Iteni wazee na wote waishio katika nchi waende katika nyumba ya Bwana Mungu wenu, wakamlilie Bwana.
Je, chakula hakikukatiliwa mbali mbele ya macho yetu: furaha na shangwe kutoka nyumba ya Mungu wetu?
Mbegu zinakauka chini ya mabonge ya udongo. Ghala zimeachwa katika uharibifu, ghala za nafaka zimebomolewa, kwa maana hakuna nafaka.
Jinsi gani ngʼombe wanavyolia! Makundi ya mifugo yanahangaika kwa sababu hawana malisho; hata makundi ya kondoo yanateseka.
Kwako, Ee Bwana, naita, kwa kuwa moto umeteketeza malisho ya mbugani na miali ya moto imeunguza miti yote shambani.