Kwa kuwa hakika ingekuwa nzito kuliko mchanga wa bahari zote, kwa hiyo si ajabu maneno yangu yamekuwa ya haraka.
Mishale ya Mwenyezi iko ndani yangu, roho yangu inakunywa sumu yake; vitisho vya Mungu vimejipanga dhidi yangu.
Ndipo bado ningekuwa na hii faraja, furaha yangu katika maumivu makali: kwamba sikuwa nimeyakana maneno yake yeye Aliye Mtakatifu.
“Ninazo nguvu gani, hata niendelee kutumaini? Matazamio yangu ya mbele ni nini, hata niendelee kuwa mvumilivu?
Je, ninao uwezo wowote wa kujisaidia mimi mwenyewe, wakati ambapo mafanikio yamefukuziwa mbali nami?
“Mtu anayekata tamaa angetazamia moyo wa kujitoa wa rafiki zake, hata kama akiacha uchaji wa Mwenyezi.
Wamedhikika, kwa sababu walikuwa na matumaini; wanafika huko, lakini wanahuzunika kwa kukosa walichotarajia.