“Kwa nini Mwenyezi asiweke nyakati kwa ajili ya hukumu? Kwa nini wale wamjuao wazitafute siku kama hizo bila mafanikio?
Kama punda-mwitu jangwani, maskini huzunguka katika kazi zao za kutafuta chakula; mahali palipo jangwa huwapa chakula cha watoto wao.
Kilio cha huzuni cha wanaokufa kinapaa kutoka mjini, nazo nafsi za waliojeruhiwa zinalilia msaada. Lakini Mungu hamlaumu mtu yeyote kwa kutenda mabaya.
Wakati mwanga wa mchana unapotoweka, muuaji huinuka naye huwaua maskini na mhitaji; wakati wa usiku hunyemelea kama mwizi.
Jicho la mzinzi hungojea wakati wa giza, naye hufikiri, ‘Hakuna jicho litakaloniona,’ naye huuficha uso wake.
Katika giza, huvunja majumba, lakini wakati wa mchana hujifungia ndani; hawataki kufanya lolote nuruni.
“Lakini wao ni povu juu ya maji; sehemu yao juu ya nchi imelaaniwa, hivyo hakuna hata mmoja aendaye kwenye shamba la mizabibu.
Kama vile joto na hari vinyakuavyo theluji iliyoyeyuka, ndivyo kuzimu kuwanyakuavyo waliotenda dhambi.
Tumbo lililowazaa huwasahau, nao huwa karamu ya mabuu; watu waovu hawakumbukwi tena, lakini huvunjika kama mti.
Kwa kitambo kidogo hutukuka, hatimaye hutoweka; hushushwa na kukusanywa kama wengine wote, hukatwa kama masuke ya nafaka.