“Pandeni na kushuka katika mitaa ya Yerusalemu, tazameni pande zote na mtafakari, tafuteni katika viwanja vyake. Kama mtaweza kumpata hata mtu mmoja tu atendaye kwa uaminifu na kutafuta kweli, nitausamehe mji huu.
Ee Bwana, je, macho yako hayaitafuti kweli? Uliwapiga, lakini hawakusikia maumivu, uliwapondaponda, lakini walikataa maonyo. Walifanya nyuso zao kuwa ngumu kuliko jiwe nao walikataa kutubu.
Ndipo nikasema, “Hawa ni maskini tu; wao ni wapumbavu, kwa maana hawaijui njia ya Bwana, sheria ya Mungu wao.
Kwa hiyo nitakwenda kwa viongozi na kuzungumza nao, hakika wao wanaijua njia ya Bwana, sheria ya Mungu wao.” Lakini kwa nia moja nao pia walikuwa wameivunja nira na kuvivunja vifungo.
Kwa hiyo simba kutoka mwituni atawashambulia, mbwa mwitu kutoka jangwani atawaangamiza, chui atawavizia karibu na miji yao, ili kumrarua vipande vipande yeyote atakayethubutu kutoka nje, kwa maana maasi yao ni makubwa, na kukengeuka kwao kumekuwa ni kwingi.
“Kwa nini niwasamehe? Watoto wenu wameniacha na kuapa kwa miungu ambayo si miungu. Niliwapatia mahitaji yao yote, lakini bado wamefanya uzinzi na kusongana katika nyumba za makahaba.
Wamelishwa vizuri, kama farasi waume wenye tamaa nyingi, kila mmoja akimlilia mke wa mwanaume mwingine.
“Piteni katika mashamba yake ya mizabibu na kuyaharibu, lakini msiangamize kabisa. Pogoeni matawi yake, kwa kuwa watu hawa sio wa Bwana.
Wamedanganya kuhusu Bwana. Wamesema, “Yeye hatafanya jambo lolote! Hakuna dhara litakalotupata; kamwe hatutaona upanga wala njaa.
Kwa hiyo hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenye Nguvu Zote: “Kwa sababu watu hawa wamesema maneno haya, nitayafanya maneno yangu vinywani mwenu kuwa moto, na watu hawa wawe kuni zinazoliwa na huo moto.
Ee nyumba ya Israeli,” asema Bwana, “Ninaleta taifa toka mbali dhidi yako, taifa la kale na linaloendelea kudumu, taifa ambalo lugha yao huijui, wala msemo wao huwezi kuuelewa.
Watayaangamiza mazao yenu na chakula chenu, wataangamiza wana wenu na mabinti zenu; wataangamiza makundi yenu ya kondoo na ya ngʼombe, wataangamiza mizabibu yenu na mitini yenu. Kwa upanga wataangamiza miji yenye maboma mliyoitumainia.
“Nao watu watakapouliza, ‘Kwa nini Bwana, Mungu wetu ametufanyia mambo haya yote?’ utawaambia, ‘Kama vile mlivyoniacha mimi na kutumikia miungu migeni katika nchi yenu wenyewe, ndivyo sasa mtakavyowatumikia wageni katika nchi ambayo si yenu.’
Sikieni hili, enyi watu wapumbavu, msio na akili, mlio na macho lakini hamwoni, mlio na masikio lakini hamsikii:
Je, haiwapasi kuniogopa mimi?” asema Bwana. “Je, haiwapasi kutetemeka mbele zangu? Niliufanya mchanga kuwa mpaka wa bahari, kizuizi cha milele ambacho haiwezi kupita. Mawimbi yanaweza kuumuka, lakini hayawezi kuupita; yanaweza kunguruma, lakini hayawezi kuuvuka.
Wao hawaambiani wenyewe, ‘Sisi na tumwogope Bwana Mungu wetu, anayetupatia mvua za masika na za vuli kwa majira yake, anayetuhakikishia majuma ya mavuno kwa utaratibu.’
“Miongoni mwa watu wangu wamo walio waovu wanaovizia kama watu wanaotega ndege, na kama wale wanaoweka mitego kuwakamata watu.
wamenenepa na kunawiri. Matendo yao maovu hayana kikomo; hawatetei mashauri ya yatima wapate kushinda, hawatetei haki za maskini.