Bwana akaniambia, “Chukua gombo kubwa, uandike juu yake kwa kalamu ya kawaida jina: Maher-Shalal-Hash-Bazi.
Kisha nikaenda kwa nabii mke, naye akapata mimba, akazaa mwana. Kisha Bwana akaniambia, “Mwite huyo mtoto Maher-Shalal-Hash-Bazi.
Kabla mtoto hajaweza kusema ‘Baba yangu’ au ‘Mama yangu,’ utajiri wa Dameski na nyara za Samaria zitachukuliwa na mfalme wa Ashuru.”
“Kwa sababu watu hawa wamekataa maji ya Shilo yatiririkayo taratibu wakamfurahia Resini na mwana wa Remalia,
kwa hiyo Bwana yu karibu kuleta dhidi yao mafuriko makubwa ya Mto: yaani mfalme wa Ashuru na fahari yake yote. Yatafurika juu ya mifereji yake yote, yatamwagikia juu ya kingo zake zote,
na kufika hadi Yuda, yakizunguka kwa kasi juu yake, yakipita katikati na yakifika hadi shingoni. Mabawa yake yaliyokunjuliwa yatafunika upana wa nchi yako, Ee Imanueli!”
Inueni kilio cha vita, enyi mataifa, na mkavunjwevunjwe! Sikilizeni, enyi nyote nchi za mbali. Jiandaeni kwa vita, nanyi mkavunjwevunjwe! Jiandaeni kwa vita, nanyi mkavunjwevunjwe!
Wekeni mikakati yenu, lakini itashindwa; fanyeni mipango yenu, lakini haitafanikiwa, kwa maana Mungu yu pamoja nasi.
Bwana alisema nami mkono wake wenye nguvu ukiwa juu yangu, akinionya nisifuate njia za taifa hili. Akasema:
“Usiite fitina kila kitu ambacho watu hawa hukiita fitina, usiogope kile wanachokiogopa, wala usikihofu.
Bwana Mwenye Nguvu Zote ndiye peke yake ikupasaye kumheshimu kuwa mtakatifu, ndiye peke yake utakayemwogopa, ndiye peke yake utakayemhofu,
naye atakuwa mahali patakatifu; lakini kwa nyumba zote mbili za Israeli atakuwa jiwe lile linalosababisha watu kujikwaa na mwamba wa kuwaangusha. Kwa watu wa Yerusalemu, atakuwa mtego na tanzi.
Niko hapa, pamoja na watoto ambao Bwana amenipa. Sisi ni ishara na mfano wake katika Israeli, kutoka kwa Bwana Mwenye Nguvu Zote, anayeishi juu ya Mlima Sayuni.
Wakati watu wanapowaambia ninyi kutafuta ushauri kwa waaguzi na wenye kuongea na mizimu, ambao hunongʼona na kunungʼunika, je, watu wasingeuliza kwa Mungu wao? Kwa nini watake shauri kwa wafu kwa ajili ya walio hai?
Watazunguka katika nchi yote, wakiwa na dhiki na njaa. Watakapotaabika kwa njaa, watapatwa na hasira kali, nao, wakiwa wanatazama juu, watamlaani mfalme wao na Mungu wao.