“Huyu hapa mtumishi wangu, ninayemtegemeza, mteule wangu, ambaye ninapendezwa naye; nitaweka Roho yangu juu yake, naye ataleta haki kwa mataifa.
hatazimia roho wala kukata tamaa, mpaka atakaposimamisha haki juu ya dunia. Visiwa vitaweka tumaini lao katika sheria yake.”
Hili ndilo asemalo Mungu, Bwana, yeye aliyeziumba mbingu na kuzitanda, aliyeitandaza dunia na vyote vitokavyo humo, awapaye watu wake pumzi, na uzima kwa wale waendao humo:
“Mimi, Bwana, nimekuita katika haki; nitakushika mkono wako. Nitakulinda na kukufanya kuwa Agano kwa ajili ya watu na nuru kwa Mataifa,
kuwafungua macho wale wasioona, kuwaacha huru kutoka kifungoni waliofungwa jela, na kuwafungua kutoka gerezani wale wanaokaa gizani.
Tazama, mambo ya kwanza yametokea, nami natangaza mambo mapya; kabla hayajatokea nawatangazia habari zake.”
Mwimbieni Bwana wimbo mpya, sifa zake toka miisho ya dunia, ninyi mshukao chini baharini, na vyote vilivyomo ndani yake, enyi visiwa na wote wakaao ndani yake.
Jangwa na miji yake na vipaze sauti zao; makao anamoishi Kedari na yashangilie. Watu wa Sela waimbe kwa furaha, na wapige kelele kutoka vilele vya milima.
Bwana ataenda kama mtu mwenye nguvu, kama shujaa atachochea shauku yake, kwa kelele ataamsha kilio cha vita, naye atashinda adui zake.
“Kwa muda mrefu nimenyamaza kimya, nimekaa kimya na kujizuia. Lakini sasa, kama mwanamke wakati wa kujifungua, ninapiga kelele, ninatweta na kushusha pumzi.
Nitaharibu milima na vilima na kukausha mimea yako yote; nitafanya mito kuwa visiwa na kukausha mabwawa.
Nitawaongoza vipofu kwenye njia ambayo hawajaijua, kwenye mapito wasiyoyazoea nitawaongoza; nitafanya giza kuwa nuru mbele yao, na kufanya mahali palipoparuza kuwa laini. Haya ndiyo mambo nitakayofanya; mimi sitawaacha.
Lakini wale wanaotumaini sanamu, wanaoviambia vinyago, ‘Ninyi ndio miungu yetu,’ watarudishwa nyuma kwa aibu kubwa.
Ni nani aliye kipofu isipokuwa mtumishi wangu, na kiziwi kama mjumbe ninayemtuma? Ni nani aliye kipofu kama yeye aliyejitoa kwangu, aliye kipofu kama mtumishi wa Bwana?
Lakini hili ni taifa lililoibwa na kutekwa nyara, wote wamenaswa katika mashimo, au wamefichwa katika magereza. Wamekuwa nyara, wala hapana yeyote awaokoaye. Wamefanywa mateka, wala hapana yeyote asemaye, “Warudishe.”
Ni nani aliyemtoa Yakobo kuwa mateka, na Israeli kwa wateka nyara? Je, hakuwa yeye, Bwana, ambaye tumetenda dhambi dhidi yake? Kwa kuwa hawakufuata njia zake, hawakutii sheria zake.