Sema na Yerusalemu kwa upole, umtangazie kwamba kazi yake ngumu imekamilika, kwamba dhambi yake imefanyiwa fidia, kwamba amepokea kutoka mkononi mwa Bwana maradufu kwa ajili ya dhambi zake zote.
Sauti ya mtu aliaye: “Itengenezeni jangwani njia ya Bwana, nyoosheni njia kuu nyikani kwa ajili ya Mungu wetu.
Kila bonde litainuliwa, kila mlima na kilima kitashushwa; penye mabonde patanyooshwa, napo palipoparuza patasawazishwa.
Utukufu wa Bwana utafunuliwa, nao wanadamu wote watauona pamoja. Kwa maana kinywa cha Bwana kimenena.”
Sauti husema, “Piga kelele.” Nami nikasema, “Nipige kelele gani?” “Wanadamu wote ni kama majani, nao utukufu wao wote ni kama maua ya kondeni.
Wewe uletaye habari njema Sayuni, panda juu ya mlima mrefu. Wewe uletaye habari njema Yerusalemu, inua sauti yako kwa kupiga kelele, inua sauti, usiogope; iambie miji ya Yuda, “Yuko hapa Mungu wenu!”
Tazameni, Bwana Mwenyezi anakuja na nguvu, nao mkono wake ndio utawalao kwa ajili yake. Tazameni, ujira wake u pamoja naye, nayo malipo yake yanafuatana naye.
Huchunga kundi lake kama mchungaji wa mifugo: Hukusanya wana-kondoo katika mikono yake na kuwachukua karibu na moyo wake, huwaongoza taratibu wale wanyonyeshao.
Ni nani aliyepima maji ya bahari kwenye konzi ya mkono wake, au kuzipima mbingu kwa shibiri yake? Ni nani aliyeyashika mavumbi ya dunia katika kikapu, au kupima milima kwenye kipimio na vilima kwenye mizani?
Ni nani ambaye Bwana ametaka shauri kwake ili kumwelimisha, naye ni nani aliyemfundisha njia iliyo sawa? Ni nani aliyemfundisha maarifa au kumwonyesha mapito ya ufahamu?
Hakika mataifa ni kama tone ndani ya ndoo, ni kama vumbi jembamba juu ya mizani, huvipima visiwa kana kwamba vilikuwa vumbi laini.
Kwa habari ya sanamu, fundi huisubu, naye mfua dhahabu huifunika kwa dhahabu na kuitengenezea mikufu ya fedha.
Mtu aliye maskini sana asiyeweza kuleta sadaka kama hii huuchagua mti usiooza. Humtafuta fundi stadi wa kusimamisha sanamu ambayo haitatikisika.
Anakaa kwenye kiti cha enzi juu ya duara ya dunia, nao watu wakaao ndani yake ni kama panzi. Huzitandaza mbingu kama chandarua, na kuzitandaza kama hema la kuishi.
Mara baada ya kupandwa, mara baada ya kutiwa ardhini, mara baada ya kutoa mizizi yao ardhini, ndipo huwapulizia nao wakanyauka, nao upepo wa kisulisuli huwapeperusha kama makapi.
Inueni macho yenu mtazame mbinguni: Ni nani aliyeumba hivi vyote? Ni yeye aletaye nje jeshi la nyota moja baada ya nyingine na kuziita kila moja kwa jina lake. Kwa sababu ya uweza wake mkuu na nguvu zake kuu, hakuna hata mojawapo inayokosekana.
Kwa nini unasema, ee Yakobo, nanyi ee Israeli, kulalamika, “Njia yangu imefichwa Bwana asiione, Mungu wangu hajali shauri langu?”
Je wewe, hufahamu? Je wewe, hujasikia? Bwana ni Mungu wa milele, Muumba wa miisho ya dunia. Hatachoka wala kulegea, wala hakuna hata mmoja awezaye kuupima ufahamu wake.