Kila mtu atakuwa kama kivuli cha kujificha kutokana na upepo na kimbilio kutokana na dhoruba, kama vijito vya maji jangwani na kivuli cha mwamba mkubwa katika ardhi yenye kiu.
Kwa kuwa mpumbavu hunena upumbavu, moyo wake hushughulika na uovu: Hutenda mambo yasiyo ya kumcha Mungu, na hueneza habari za makosa kuhusu Bwana; yeye huwaacha wenye njaa bila kitu, na wenye kiu huwanyima maji.
Taratibu za mtu mbaya kabisa ni ovu, hufanya mipango miovu ili kumwangamiza maskini kwa uongo, hata wakati ambapo hoja za mhitaji ni za haki.
Enyi wanawake wenye kuridhika sana, amkeni na mnisikilize. Enyi binti mnaojisikia kuwa salama, sikieni lile ninalotaka kuwaambia!
Muda zaidi kidogo ya mwaka mmoja, ninyi mnaojisikia salama mtatetemeka, mavuno ya zabibu yatakoma na mavuno ya matunda hayatakuwepo.
Tetemekeni, enyi wanawake wenye kuridhika, tetemekeni kwa hofu, enyi binti mnaojisikia salama! Vueni nguo zenu, vaeni nguo ya gunia viunoni mwenu.
na kwa ajili ya nchi ya watu wangu, nchi ambayo miiba na michongoma imemea: naam, ombolezeni kwa ajili ya nyumba zote za furaha na kwa ajili ya mji huu wenye kufanya sherehe.
Ngome itaachwa, mji wenye kelele nyingi utahamwa, ngome ndani ya mji na mnara wa ulinzi vitakuwa ukiwa milele, mahali pazuri pa punda na malisho ya makundi ya kondoo,
mpaka Roho amwagwe juu yetu kutoka juu, nalo jangwa kuwa shamba lenye rutuba, na shamba lenye rutuba kuwa kama msitu.
Watu wangu wataishi katika makao ya mahali pa amani, katika nyumba zilizo salama, katika mahali pa kupumzika pasipo na usumbufu.