Katika siku ile, wimbo huu utaimbwa katika nchi ya Yuda: Tuna mji ulio na nguvu, Mungu huufanya wokovu kuwa kuta zake na maboma yake.
Huwashusha wale wajikwezao, huushusha chini mji wenye kiburi, huushusha hadi ardhini na kuutupa chini mavumbini.
Naam, Bwana, tukienenda katika sheria zako, twakungojea wewe, jina lako na sifa zako ndizo shauku za mioyo yetu.
Nafsi yangu yakutamani wakati wa usiku, wakati wa asubuhi roho yangu yakuonea shauku. Wakati hukumu zako zinapokuja juu ya dunia, watu wa ulimwengu hujifunza haki.
Ingawa neema yaonyeshwa kwa waovu, hawajifunzi haki, hata katika nchi ya unyofu huendelea kutenda mabaya wala hawazingatii utukufu wa Bwana.
Ee Bwana, mkono wako umeinuliwa juu, lakini hawauoni. Wao na waone wivu wako kwa ajili ya watu wako tena waaibishwe, moto uliowekwa akiba kwa ajili ya adui zako na uwateketeze.
Bwana, unaamuru amani kwa ajili yetu, yale yote tuliyoweza kuyakamilisha ni wewe uliyetenda kwa ajili yetu.
Ee Bwana, Mungu wetu, mabwana wengine zaidi ya wewe wametutawala, lakini jina lako pekee ndilo tunaloliheshimu.
Wao sasa wamekufa, wala hawako tena hai, roho za waliokufa hazitarudi tena. Uliwaadhibu na kuwaangamiza, umefuta kumbukumbu lao lote.
Umeliongeza hilo taifa, Ee Bwana, umeliongeza hilo taifa. Umejipatia utukufu kwa ajili yako mwenyewe, umepanua mipaka yote ya nchi.
Kama mwanamke mwenye mimba aliyekaribia kuzaa anavyogaagaa na kulia kwa ajili ya maumivu yake, ndivyo tulivyokuwa mbele zako, Ee Bwana.
Tulikuwa na mimba, tuligaagaa kwa maumivu, lakini tulizaa upepo. Hatukuleta wokovu duniani, hatujazaa watu katika ulimwengu huu.
Lakini wafu wenu wataishi, nayo miili yao itafufuka. Ninyi mnaokaa katika mavumbi, amkeni mkapige kelele kwa furaha. Umande wenu ni kama umande wa asubuhi, dunia itawazaa wafu wake.
Nendeni, watu wangu, ingieni vyumbani mwenu na mfunge milango nyuma yenu, jificheni kwa kitambo kidogo mpaka ghadhabu yake ipite.