Neno kuhusu Misri: Tazama, Bwana amepanda juu ya wingu liendalo kwa haraka naye anakuja Misri. Sanamu za Misri zinatetemeka mbele yake, nayo mioyo ya Wamisri inayeyuka ndani yao.
“Nitamchochea Mmisri dhidi ya Mmisri, ndugu atapigana dhidi ya ndugu, jirani dhidi ya jirani, mji dhidi ya mji, ufalme dhidi ya ufalme.
Wamisri watakufa moyo, na nitaibatilisha mipango yao. Watatafuta ushauri kwa sanamu na kwa roho za waliokufa, kwa waaguzi na kwa wale waongeao na mizimu.
Nitawatia Wamisri mikononi mwa bwana mkatili na mfalme mkali atatawala juu yao,” asema Bwana, Bwana Mwenye Nguvu Zote.
pia mimea iliyoko kando ya Mto Naili, pale mto unapomwaga maji baharini. Kila shamba lililopandwa kando ya Mto Naili litakauka, litapeperushwa na kutoweka kabisa.
Wale watu wafanyao kazi ya kitani kilichochambuliwa watakata tamaa, wafumaji wa kitani safi watavunjika moyo.
Maafisa wa Soani ni wapumbavu kabisa, washauri wa Farao wenye busara wanatoa ushauri wa kijinga. Unawezaje kumwambia Farao, “Mimi ni mmojawapo wa watu wenye hekima, mwanafunzi wa wafalme wa zamani”?
Wako wapi sasa watu wako wenye hekima? Wao wakuonyeshe na kukufahamisha ni nini Bwana Mwenye Nguvu Zote amepanga dhidi ya Misri.
Maafisa wa Soani wamekuwa wapumbavu, viongozi wa Memfisi wamedanganyika, walio mawe ya pembe ya taifa lake wameipotosha Misri.
Bwana amewamwagia roho ya kizunguzungu; wanaifanya Misri iyumbayumbe katika yale yote inayoyafanya, kama vile mlevi ayumbayumbavyo katika kutapika kwake.
Katika siku ile Wamisri watakuwa kama wanawake. Watatetemeka kwa hofu mbele ya mkono wa Bwana Mwenye Nguvu Zote anaoinua dhidi yao.
Nayo nchi ya Yuda itawatia hofu Wamisri, kila mmoja atakayetajiwa Yuda ataingiwa na hofu, kwa sababu ya kile ambacho Bwana Mwenye Nguvu Zote anapanga dhidi yao.
Katika siku hiyo miji mitano ya Misri, itazungumza lugha ya Kanaani, na kuapa kumtii Bwana Mwenye Nguvu Zote. Mji mmojawapo utaitwa Mji wa Uharibifu.
Katika siku hiyo patakuwepo madhabahu ya Bwana katikati ya Misri na mnara wa kumbukumbu kwa Bwana kwenye mpaka wa Misri.
Itakuwa alama na ushahidi kwa ajili ya Bwana Mwenye Nguvu Zote katika nchi ya Misri. Watakapomlilia Bwana kwa sababu ya watesi wao, Mungu atawapelekea mwokozi na mtetezi, naye atawaokoa.
Hivyo Bwana atajijulisha mwenyewe kwa Wamisri, nao katika siku hiyo watamkubali Bwana. Wataabudu kwa kumtolea dhabihu na sadaka za nafaka, watamwekea Bwana nadhiri na kuzitimiza.
Bwana ataipiga Misri kwa tauni; atawapiga na kuwaponya. Watamgeukia Bwana, naye atayasikia maombi yao na kuwaponya.
Katika siku hiyo kutakuwepo na njia kuu kutoka Misri hadi Ashuru. Waashuru watakwenda Misri, na Wamisri watakwenda Ashuru. Wamisri na Waashuru wataabudu pamoja.