kuwanyima maskini haki zao na kuzuilia haki za watu wangu walioonewa, kuwafanya wajane mawindo yao na kuwanyangʼanya yatima.
Mtafanya nini siku ya kutoa hesabu, wakati maafa yatakapokuja kutoka mbali? Mtamkimbilia nani awape msaada? Mtaacha wapi mali zenu?
Hakutasalia kitu chochote, isipokuwa kujikunyata miongoni mwa mateka, au kuanguka miongoni mwa waliouawa. Hata kwa haya yote, hasira yake haijageukia mbali, mkono wake bado umeinuliwa juu.
Ninamtuma dhidi ya taifa lisilomjua Mungu, ninamtuma dhidi ya taifa linalonikasirisha, kukamata mateka na kunyakua nyara, pia kuwakanyaga chini kama matope ya barabarani.
Lakini hili silo analokusudia, hili silo alilo nalo akilini; kusudi lake ni kuangamiza, kuyakomesha mataifa mengi.
Kama vile mkono wangu ulivyotwaa falme za sanamu, falme ambazo vinyago vyao vilizidi vile vya Yerusalemu na Samaria:
Bwana atakapokuwa amemaliza kazi yake yote dhidi ya Mlima Sayuni na Yerusalemu, atasema, “Nitamwadhibu mfalme wa Ashuru kwa ajili ya majivuno ya ukaidi wa moyo wake na kutazama kwa macho yenye dharau.”
Kwa kuwa anasema: “ ‘Kwa nguvu za mkono wangu nimefanya hili, kwa hekima yangu, kwa sababu nina ufahamu. Niliondoa mipaka ya mataifa, niliteka nyara hazina zao, kama yeye aliye shujaa niliwatiisha wafalme wao.
Kama mtu atiavyo mkono kwenye kiota, ndivyo mkono wangu ulivyochukua utajiri wa mataifa; kama watu wakusanyavyo mayai yaliyoachwa, ndivyo nilivyokusanya nchi zote; wala hakuna hata mmoja aliyepiga bawa au kufungua kinywa chake kutoa mlio.’ ”
Je, shoka laweza kujigamba kuwa na nguvu zaidi kuliko yule anayelitumia, au msumeno kujisifu dhidi ya yule anayeutumia? Ni kana kwamba fimbo ingeweza kumwinua yeye aichukuaye, au mkongojo ungemwinua mwenye kuutumia!
Kwa hiyo Bwana, Bwana Mwenye Nguvu Zote, atatuma ugonjwa wa kudhoofisha kwa askari wake walio hodari, katika fahari yake moto utawaka kama mwali wa moto.
Nuru ya Israeli itakuwa moto, Aliye Mtakatifu wao mwali wa moto; katika siku moja utaunguza na kuteketeza miiba na michongoma yake.
Fahari ya misitu yake na mashamba yenye rutuba utateketeza kabisa, kama vile mtu mgonjwa adhoofikavyo.
Katika siku ile, mabaki ya Israeli, walionusurika wa nyumba ya Yakobo, hawatamtegemea tena yeye aliyewapiga, lakini watamtegemea kwa kweli Bwana Aliye Mtakatifu wa Israeli.
Ingawa watu wako, ee Israeli, ni wengi kama mchanga wa pwani, ni mabaki yao tu watakaorudi. Maangamizi yamekwisha amriwa, ni mengi tena ni haki.
Kwa hiyo, hili ndilo Bwana, Bwana Mwenye Nguvu Zote asemalo: “Enyi watu wangu mkaao Sayuni, msiwaogope Waashuru, wanaowapiga ninyi kwa fimbo na kuinua rungu dhidi yenu, kama Misri ilivyofanya.
Bado kitambo kidogo sana hasira yangu dhidi yenu itakoma, na ghadhabu yangu itaelekezwa kwenye maangamizi yao.”
Bwana Mwenye Nguvu Zote atawachapa kwa mjeledi, kama alivyowapiga Wamidiani katika mwamba wa Orebu, naye atainua fimbo yake juu ya maji, kama alivyofanya huko Misri.
Katika siku hiyo mzigo wao utainuliwa kutoka mabegani mwenu, na nira yao kutoka shingoni mwenu; nira itavunjwa kwa sababu ya kutiwa mafuta.
Wanavuka kivukoni, nao wanasema, “Tutapiga kambi huko Geba usiku kucha.” Rama inatetemeka; Gibea ya Sauli inakimbia.
Siku hii ya leo watasimama Nobu; watatikisa ngumi zao kwa mlima wa Binti Sayuni, kwa kilima cha Yerusalemu.
Tazama, Bwana, Bwana Mwenye Nguvu Zote, atayakata matawi kwa nguvu kuu. Miti mirefu sana itaangushwa, ile mirefu itashushwa chini.