“Wekeni tarumbeta midomoni mwenu! Tai yuko juu ya nyumba ya Bwana kwa sababu watu wamevunja Agano langu, wameasi dhidi ya sheria yangu.
Wanaweka wafalme bila idhini yangu, wamechagua wakuu bila kibali changu. Kwa fedha zao na dhahabu wamejitengenezea sanamu kwa ajili ya maangamizi yao wenyewe.
Ee Samaria, tupilieni mbali sanamu yenu ya ndama! Hasira yangu inawaka dhidi yao. Watakuwa najisi mpaka lini?
Zimetoka katika Israeli! Ndama huyu: ametengenezwa na fundi, si Mungu. Atavunjwa vipande vipande, yule ndama wa Samaria.
“Wanapanda upepo na kuvuna upepo wa kisulisuli. Bua halina suke, halitatoa unga. Kama lingetoa nafaka, wageni wangeila yote.
Kwa kuwa wamepanda kwenda Ashuru kama punda-mwitu anayetangatanga peke yake. Efraimu amejiuza mwenyewe kwa wapenzi.
Ingawa wamejiuza wenyewe miongoni mwa mataifa, sasa nitawakusanya pamoja. Wataanza kudhoofika chini ya uonevu wa mfalme mwenye nguvu.
“Ingawa Efraimu alijenga madhabahu nyingi kwa ajili ya sadaka za dhambi, hizi zimekuwa madhabahu za kufanyia dhambi.
Nimeandika kwa ajili yao mambo mengi kuhusu sheria yangu, lakini wameziangalia kama kitu cha kigeni.
Wanatoa dhabihu nilizopewa mimi nao wanakula hiyo nyama, lakini Bwana hapendezwi nao. Sasa ataukumbuka uovu wao na kuadhibu dhambi zao: Watarudi Misri.