“Njooni, tumrudie Bwana. Ameturarua vipande vipande lakini atatuponya; ametujeruhi lakini atatufunga majeraha yetu.
Tumkubali Bwana, tukaze kumkubali yeye. Kutokea kwake ni hakika kama vile kuchomoza kwa jua; atatujia kama mvua za masika, kama vile mvua za vuli ziinyweshavyo nchi.”
“Nifanye nini nawe, Efraimu? Nifanye nini nawe, Yuda? Upendo wako ni kama ukungu wa asubuhi, kama umande wa alfajiri utowekao.
Kwa hiyo ninawakata ninyi vipande vipande kwa kutumia manabii wangu; nimewaua ninyi kwa maneno ya kinywa changu, hukumu zangu zinawaka kama umeme juu yenu.
Kama wanyangʼanyi wamviziavyo mtu, ndivyo magenge ya makuhani wafanyavyo; wanaulia watu kwenye njia iendayo Shekemu, wakifanya uhalifu wa aibu.
Nimeona jambo la kutisha katika nyumba ya Israeli. Huko Efraimu amejitolea kwa ukahaba na Israeli amenajisika.