Ee Bwana, hata lini nitakuomba msaada, lakini wewe husikilizi? Au kukulilia, “Udhalimu!” Lakini hutaki kuokoa?
Kwa nini unanifanya nitazame dhuluma? Kwa nini unavumilia makosa? Uharibifu na udhalimu viko mbele yangu; kuna mabishano na mapambano kwa wingi.
Kwa hiyo sheria imepotoshwa, nayo haki haipo kabisa. Waovu wanawazunguka wenye haki, kwa hiyo haki imepotoshwa.
“Yatazame mataifa, uangalie na ushangae kabisa. Kwa sababu katika siku zako nitafanya kitu ambacho hungeamini, hata kama ungeambiwa.
Nitawainua Wakaldayo, watu hao wakatili na wenye haraka, ambao hupita dunia yote kuteka mahali pa kuishi pasipo pao wenyewe.
Farasi wao ni wepesi kuliko chui, na wakali kuliko mbwa mwitu wakati wa machweo. Askari wapanda farasi wao huenda mbio; waendesha farasi wao wanatoka mbali. Wanaruka kasi kama tai ili kurarua;
wote wanakuja tayari kwa fujo. Makundi yao ya wajeuri yanasonga mbele kama upepo wa jangwani, na kukusanya wafungwa kama mchanga.
Wanawabeza wafalme, na kuwadhihaki watawala. Wanaicheka miji yote iliyozungushiwa maboma; wanafanya malundo ya udongo na kuiteka hiyo miji.
Ee Bwana, je, wewe sio wa tangu milele? Mungu wangu, Uliye Mtakatifu wangu, hatutakufa. Ee Bwana, umewachagua wao ili watekeleze hukumu; Ee Mwamba, umewaamuru watuadhibu.
Macho yako ni safi mno hata yasiweze kuutazama uovu, wala huwezi kuvumilia makosa. Kwa nini basi unawavumilia wadanganyifu? Kwa nini unakuwa kimya wakati waovu wanawameza wale wenye haki kuliko wao wenyewe?
Adui mwovu anawavuta wote kwa ndoana, anawakamata katika wavu wake, anawakusanya katika juya lake; kwa hiyo anashangilia na anafurahi.
Kwa hiyo anatoa kafara kwa wavu wake, na kuchoma uvumba kwa juya lake, kwa kuwa kwa wavu wake anaishi kwa starehe, na anafurahia chakula kizuri.