Lile nisemalo ni kwamba wakati wote mrithi bado ni mtoto, hana tofauti na mtumwa, ingawa ndiye mmiliki wa mali yote.
Vivyo hivyo na sisi, tulipokuwa bado watoto wadogo, tulikuwa utumwani chini ya taratibu za kawaida za ulimwengu.
Lakini ulipowadia utimilifu wa wakati, Mungu alimtuma Mwanawe, ambaye alizaliwa na mwanamke, akazaliwa chini ya sheria,
kusudi awakomboe wale waliokuwa chini ya sheria, ili tupate kupokea zile haki kamili za kufanywa watoto wa Mungu.
Kwa sababu ninyi ni watoto wa Mungu, Mungu amemtuma Roho wa Mwanawe mioyoni mwetu, anayelia, “Abba, Baba.”
Kwa hiyo, wewe si mtumwa tena, bali ni mtoto, kwa kuwa wewe ni mtoto, Mungu amekufanya wewe pia kuwa mrithi kwa kupitia Kristo.
Lakini sasa kwa kuwa mmemjua Mungu, au zaidi mmejulikana na Mungu, inakuwaje mnarejea tena katika zile kanuni za kwanza zenye udhaifu na upungufu? Mnataka ziwafanye tena watumwa?
Ndugu zangu, nawasihi mwe kama mimi, kwa sababu mimi nimekuwa kama ninyi. Hamkunitendea jambo lolote baya.
Ingawa hali yangu iliwatia majaribuni, hamkunidharau wala kunidhihaki, bali mlinikaribisha kama malaika wa Mungu, kama vile Kristo Yesu.
Ile hali ya furaha mliyokuwa nayo imekwenda wapi? Naweza kushuhudia kwamba, kama ingewezekana mngengʼoa macho yenu na kunipa mimi.
Hao wana shauku ya kuwapata lakini si kwa kusudi zuri. Wanachotaka ni kuwatenga mbali nasi, ili ninyi mpate kuwaonea wao shauku.
Watoto wangu wapendwa, ambao kwa mara nyingine ninawaonea utungu, ninatamani kwamba Kristo aumbike ndani yenu.
Natamani kama ningekuwa pamoja nanyi sasa, pengine ningebadilisha sauti yangu. Kwa maana nina wasiwasi kwa ajili yenu.
Kwa maana imeandikwa kwamba Abrahamu alikuwa na wana wawili, mmoja wa mwanamke mtumwa na wa pili wa mwanamke huru.
Lakini, mtoto wa mwanamke mtumwa alizaliwa kwa mapenzi ya mwili, na yule mwingine wa mwanamke huru alizaliwa kutokana na ahadi ya Mungu.
Mambo haya yanaweza kuchukuliwa kama mfano. Kwa maana hao wanawake wawili ni mfano wa maagano mawili: Agano la kwanza, ni lile lililofanyika katika Mlima Sinai, lizaalo watoto wa utumwa. Hili ndilo huyo Hagari.
Basi Hagari anawakilisha Mlima Sinai ulioko Arabuni, na unafanana na Yerusalemu ya sasa ambayo iko utumwani pamoja na watoto wake.
Kwa maana imeandikwa: “Furahi, ewe mwanamke tasa, wewe usiyezaa; paza sauti, na kuimba kwa furaha, wewe usiyepatwa na utungu wa kuzaa; kwa maana watoto wa mwanamke aliyeachwa ukiwa ni wengi kuliko wa mwanamke mwenye mume.”
Lakini, kama vile ilivyokuwa siku zile yule aliyezaliwa kwa mwili alivyomchokoza yule aliyezaliwa kwa Roho, ndivyo ilivyo hata sasa.
Lakini Maandiko yasemaje? “Mwondoe mwanamke mtumwa pamoja na mwanawe, kwa sababu mwana wa mwanamke mtumwa kamwe hatarithi pamoja na mwana wa aliye huru.”