Hawa ndio viongozi wa jamaa pamoja na wale walioandikwa ambao walikuja pamoja nami kutoka Babeli wakati wa utawala wa Mfalme Artashasta:
wa wazao wa Finehasi, alikuwa Gershoni; wa wazao wa Ithamari, alikuwa Danieli; wa wazao wa Daudi, alikuwa Hatushi
wa wazao wa Shekania; wa wazao wa Paroshi, alikuwa Zekaria, na watu 150 walioandikishwa pamoja naye;
wa wazao wa Adonikamu, hawa walikuwa wa mwisho ambao majina yao ni Elifeleti, Yeueli, Shemaya na wanaume 60 pamoja nao;
Niliwakusanya kwenye mto utiririkao kuelekea Ahava, nasi tukapiga kambi pale siku tatu. Wakati nilipokagua kati ya watu na makuhani, sikuwapata Walawi.
Basi niliwaita Eliezeri, Arieli, Shemaya, Elnathani, Yaribu, Elnathani, Nathani, Zekaria na Meshulamu waliokuwa viongozi na Yoyaribu na Elnathani waliokuwa wasomi,
nikawatuma kwa Ido kiongozi huko Kasifia. Niliwaambia watakayomwambia Ido na ndugu zake, watumishi wa Hekalu huko Kasifia, ili waweze kutuletea wahudumu kwa ajili ya nyumba ya Mungu wetu.
Kwa sababu mkono wa neema wa Mungu wetu ulikuwa juu yetu, walituletea Sherebia, mtu mwenye uwezo kutoka wazao wa Mahli mwana wa Lawi, mwana wa Israeli, na wana wa Sherebia pamoja na ndugu zao wanaume kumi na wanane.
Naye Hashabia, pamoja na Yeshaya kutoka wazao wa Merari na ndugu zake na wapwa wake wanaume ishirini.
Vilevile walileta watumishi wa Hekalu 220, kikundi ambacho Daudi na maafisa walikuwa wamekiweka kusaidia Walawi. Wote walikuwa wameorodheshwa kwa majina.
Kando ya Mto Ahava, hapo nilitangaza kufunga, ili tujinyenyekeshe mbele za Mungu wetu na kumwomba kwa ajili ya kutujalia safari ya amani sisi na watoto wetu, pamoja na mali zetu zote.
Niliona aibu kumwomba mfalme askari na wapanda farasi wa kutulinda njiani kutokana na adui zetu, kwa sababu tulikwisha kumwambia mfalme, “Mkono wa neema wa Mungu wetu uko juu ya kila mmoja anayemtafuta, lakini hasira yake kubwa ni dhidi ya wote wamwachao.”
Kisha niliwatenga viongozi wa makuhani kumi na wawili, pamoja na Sherebia, Hashabia na ndugu zao kumi,
nami nikawapimia fedha, dhahabu na vifaa ambavyo mfalme, washauri wake, maafisa wake na Israeli wote waliokuwepo walikuwa wamevitoa sadaka kwa ajili ya nyumba ya Mungu wetu.
Niliwapimia talanta 650 za fedha, vifaa vingine vya fedha vya uzito wa talanta mia moja, talanta mia moja za dhahabu,
mabakuli ishirini ya dhahabu ya thamani ya darkoni elfu moja, na vyombo viwili vya shaba iliyosuguliwa, ya thamani kama dhahabu.
Niliwaambia, “Ninyi pamoja na vyombo hivi ni wakfu kwa Bwana. Fedha na dhahabu ni sadaka ya hiari kwa Bwana, Mungu wa baba zenu.
Vilindeni kwa uangalifu mpaka mtakapovipima ndani ya vyumba vya nyumba ya Bwana katika Yerusalemu mbele ya makuhani, viongozi na Walawi pamoja na wakuu wa jamaa za Israeli.”
Ndipo makuhani na Walawi wakapokea fedha, dhahabu na vyombo vilivyowekwa wakfu ambavyo vilipimwa na kupelekwa katika nyumba ya Mungu wetu mjini Yerusalemu.
Tulianza safari kutoka Mto Ahava kwenda Yerusalemu kwenye siku ya kumi na mbili ya mwezi wa kwanza. Mkono wa Mungu wetu ulikuwa juu yetu, naye njiani alitulinda dhidi ya adui na wanyangʼanyi.
Katika siku ya nne, ndani ya nyumba ya Mungu wetu, tulipima fedha, dhahabu na vyombo vilivyowekwa wakfu, tukakabidhi mikononi mwa kuhani Meremothi mwana wa Uria. Eleazari mwana wa Finehasi alikuwa pamoja naye, pia walikuwako Walawi wawili, Yozabadi mwana wa Yeshua na Noadia mwana wa Binui.
Kisha mateka waliokuwa wamerudi kutoka utumwani wakatoa sadaka za kuteketezwa kwa moto kwa Mungu wa Israeli: mafahali kumi na wawili kwa ajili ya Israeli wote, kondoo dume tisini na sita, wana-kondoo sabini na saba na mbuzi dume kumi na wawili kuwa sadaka ya dhambi. Hii yote ilikuwa sadaka ya kuteketezwa kwa moto kwa Bwana.