na useme: ‘Hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: Mimi ni kinyume nawe, ee mlima Seiri, nami nitanyoosha mkono wangu dhidi yako na kukufanya ukiwa na usiyekaliwa na watu wala kulimika.
“ ‘Kwa sababu ulificha moyoni uadui wa siku nyingi nawe ukawatoa Waisraeli wauawe kwa upanga wakati wa maafa yao, wakati adhabu yake ilipofikia kilele chake,
kwa hiyo hakika kama niishivyo, asema Bwana Mwenyezi, nitakutia katika umwagaji damu nao utakufuatia. Kwa kuwa hakuchukia kumwaga damu, kumwaga damu kutakufuatia.
Nitaufanya Mlima Seiri ukiwa na usiokaliwa na watu wala kulimika na kuukatilia mbali na wote wanaokuja na wanaokwenda.
Nitaijaza milima yenu kwa watu wake waliouawa, wale waliouawa kwa upanga wataanguka juu ya vilima vyako na katika mabonde yako na katika makorongo yako yote.
“ ‘Kwa sababu umesema, “Mataifa haya mawili na nchi hizi zitakuwa zetu nasi tutazimiliki,” ingawa hata mimi Bwana nilikuwa huko,
kwa hiyo hakika kama niishivyo, asema Bwana Mwenyezi, nitakutenda kwa kadiri ya hasira na wivu uliouonyesha katika chuki yako juu yao nami nitafanya nijulikane miongoni mwao wakati nitakapokuhukumu.
Ndipo utakapojua kuwa Mimi Bwana nimesikia mambo yote ya dharau uliyosema dhidi ya milima ya Israeli. Ulisema, “Wamefanyika ukiwa na kutiwa mikononi mwetu tuwararue.”