wakati wa kutawanya mawe na wakati wa kukusanya mawe, wakati wa kukumbatia na wakati wa kutokumbatia,
Amefanya kila kitu kiwe kizuri kwa wakati wake. Pia ameiweka hiyo milele katika mioyo ya wanadamu, wala hawawezi kutambua kwa kina yale ambayo Mungu amefanya tangu mwanzo hadi mwisho.
Ninajua kwamba hakuna kitu bora kwa wanadamu kuliko kuwa na furaha na kutenda mema wakati wanapoishi.
Tena ni karama ya Mungu kila mtu apate kula na kunywa na kujiburudisha kwa mema katika kazi yake yote.
Ninajua kwamba kila kitu anachokifanya Mungu kitadumu milele, hakuna kinachoweza kuongezwa au kupunguzwa. Mungu hufanya hivyo ili watu wamche yeye.
Chochote kilichopo kilishakuwepo, na kitakachokuwepo kimekwishakuwepo kabla; naye Mungu huyaita yale yaliyopita yarudi tena.
Pia nikaona kitu kingine tena chini ya jua: Mahali pa kutolea hukumu, uovu ulikuwepo, mahali pa kupatia haki, uovu ulikuwepo.
Nikafikiri moyoni mwangu, “Mungu atawaleta hukumuni wote wawili wenye haki na waovu, kwa maana kutakuwako na wakati kwa ajili ya kila jambo, wakati kwa ajili ya kila tendo.”
Hatima ya mwanadamu ni kama ile ya wanyama; wote wana mwisho unaofanana: Jinsi anavyokufa mnyama, ndivyo anavyokufa mwanadamu. Wote wana pumzi inayofanana; mwanadamu hana cha zaidi kuliko mnyama. Kila kitu ni ubatili.