Mtakapokuwa mmevuka Mto Yordani na kuingia katika nchi awapayo Bwana Mungu wenu, msimamishe mawe makubwa na mkayatie lipu.
Andikeni juu yake maneno yote ya sheria hii wakati mtakapokuwa mmevuka na kuingia katika nchi awapayo Bwana Mungu wenu, nchi itiririkayo maziwa na asali, kama vile Bwana, Mungu wa baba zenu, alivyowaahidi.
Mtakapokuwa mmevuka Yordani, simamisheni mawe haya juu ya Mlima Ebali, kama ninavyowaagiza leo, mkayatie lipu.
Huko mjengeeni Bwana Mungu wenu madhabahu, madhabahu ya mawe. Msitumie kifaa chochote cha chuma juu yake.
Jengeni madhabahu ya Bwana Mungu wenu kwa mawe ya shambani, na mtoe sadaka za kuteketezwa juu yake kwa Bwana Mungu wenu.
Kisha Mose na makuhani, ambao ni Walawi, wakawaambia Israeli wote, “Nyamaza ee Israeli, sikiliza! Sasa umekuwa taifa la Bwana Mungu wako.
Mtakapovuka Mto Yordani, makabila haya yatasimama juu ya Mlima Gerizimu kubariki watu: Simeoni, Lawi, Yuda, Isakari, Yosefu na Benyamini.
Makabila haya yatasimama juu ya Mlima Ebali kwa kutamka laana: Reubeni, Gadi, Asheri, Zabuloni, Dani na Naftali.
“Alaaniwe mtu afanyaye sanamu ya kuchonga au mwenye kusubu sanamu, kitu ambacho ni chukizo kwa Bwana, kazi ya mikono ya fundi stadi, na kuisimamisha kwa siri.” Kisha watu wote watasema, “Amen!”
“Alaaniwe mtu akutanaye kimwili na mke wa baba yake, kwa maana anadharau malazi ya baba yake.” Kisha watu wote watasema, “Amen!”
“Alaaniwe mtu akutanaye kimwili na dada yake, binti wa baba yake au binti wa mama yake.” Kisha watu wote watasema, “Amen!”