Baada ya siku tano, kuhani mkuu Anania akashuka akiwa amefuatana na baadhi ya wazee pamoja na mwanasheria mmoja aitwaye Tertulo, nao wakaleta mashtaka yao dhidi ya Paulo mbele ya mtawala.
Paulo alipoitwa aingie ndani, Tertulo akaanza kutoa mashtaka akisema, “Mtukufu Feliksi, kwa muda mrefu tumefurahia amani na matengenezo mengi mazuri yamefanywa kwa ajili ya watu hawa kwa sababu ya upeo wako wa kuona mambo ya mbele.
Wakati wote na kila mahali, kwa namna yoyote, mtukufu sana Feliksi, tumeyapokea mambo haya yote kwa shukrani nyingi.
“Tumemwona mtu huyu kuwa ni msumbufu, anayechochea ghasia miongoni mwa Wayahudi duniani pote. Yeye ndiye kiongozi wa dhehebu la Wanazarayo,
na hata amejaribu kulinajisi Hekalu, hivyo tukamkamata; [tukataka kumhukumu kufuatana na sheria zetu.
akiwaamuru washtaki wake waje mbele yako: ili] kwa kumchunguza wewe mwenyewe unaweza kujua kutoka kwake mambo yote tunayomshtaki kwayo.”
Mtawala Feliksi alipompungia Paulo mkono ili ajitetee, yeye akajibu, “Najua kwamba wewe umekuwa hakimu katika taifa hili kwa miaka mingi, hivyo natoa utetezi wangu kwa furaha.
Unaweza kuhakikisha kwa urahisi kuwa hazijapita zaidi ya siku kumi na mbili tangu nilipopanda kwenda Yerusalemu kuabudu.
Hawa wanaonishtaki hawakunikuta nikibishana na mtu yeyote Hekaluni au kuchochea umati wa watu katika sinagogi au mahali pengine popote mjini.
Lakini, ninakubali kwamba mimi namwabudu Mungu wa baba zetu, mfuasi wa Njia, ile ambayo wao wanaiita dhehebu. Ninaamini kila kitu kinachokubaliana na Sheria na kile kilichoandikwa katika Manabii,
nami ninalo tumaini kwa Mungu, ambalo hata wao wenyewe wanalikubali kwamba kutakuwa na ufufuo wa wafu, kwa wenye haki na wasio na haki.
“Basi, baada ya kutokuwepo kwa miaka mingi nilikuja Yerusalemu ili kuwaletea watu wangu msaada kwa ajili ya maskini na kutoa dhabihu.
Nilikuwa nimeshatakaswa kwa taratibu za kiibada waliponikuta Hekaluni nikifanya mambo haya. Hapakuwa na umati wa watu, pamoja nami wala aliyehusika kwenye fujo yoyote.
Lakini kulikuwa na baadhi ya Wayahudi kutoka Asia, ambao wangelazimika wawepo hapa mbele yako ili watoe mashtaka kama wanalo jambo lolote dhidi yangu.
isipokuwa ni kuhusu jambo hili moja nililopiga kelele mbele yao kwamba, ‘Mimi nashtakiwa mbele yenu leo kwa sababu ya ufufuo wa wafu.’ ”
Basi Feliksi ambaye alikuwa anafahamu vizuri habari za Njia ile, akaahirisha shauri lile kwa maelezo yake akisema, “Wakati jemadari Lisia atakapoteremka huku, nitaamua shauri lako.”
Ndipo akaamuru kiongozi wa askari amweke chini ya ulinzi lakini ampe uhuru na kuwaruhusu rafiki zake wamhudumie.
Baada ya siku kadhaa, Feliksi alikuja pamoja na Drusila mkewe, ambaye alikuwa Myahudi. Alituma aitiwe Paulo, naye akamsikiliza alipokuwa akinena juu ya imani katika Kristo Yesu.
Naye Paulo alipokuwa akinena juu ya haki, kuwa na kiasi na juu ya hukumu ijayo, Feliksi aliingiwa na hofu na kusema, “Hiyo yatosha sasa! Waweza kuondoka. Nitakapokuwa na wasaa nitakuita.”
Wakati huo Feliksi alitazamia kwamba Paulo angempa rushwa. Hivyo akawa anamwita mara kwa mara na kuzungumza naye.