Hii ndiyo mara ya tatu mimi kuja kwenu. “Shtaka lolote lazima lithibitishwe na mashahidi wawili au watatu.”
Nimekwisha kuwaonya nilipokuwa pamoja nanyi mara ya pili. Sasa narudia wakati sipo, kwamba nikija tena sitawahurumia wale waliokuwa wametenda dhambi hapo awali na wengine wote,
kwa kuwa mnadai uthibitisho kwamba Kristo anazungumza kwa kunitumia mimi. Yeye si dhaifu katika kushughulika nanyi, bali ana nguvu kati yenu.
Kwa kuwa alisulubiwa katika udhaifu, lakini anaishi kwa nguvu za Mungu. Vivyo hivyo, sisi tu dhaifu kupitia kwake, lakini katika kuwashughulikia ninyi tutaishi pamoja naye kwa nguvu za Mungu.
Jichunguzeni wenyewe mwone kama mnaishi katika imani. Jipimeni wenyewe. Je, hamtambui ya kuwa Yesu Kristo yumo ndani yenu? Kama sivyo, basi, mmeshindwa kufikia kipimo hicho!
Lakini tunamwomba Mungu msije mkatenda kosa lolote, si ili sisi tuonekane kuwa tumeshinda hilo jaribio, bali ili ninyi mtende lililo haki, hata kama tutaonekana kuwa tumeshindwa.
Tunafurahi wakati wowote sisi tunapokuwa dhaifu, lakini ninyi mkawa na nguvu. Nayo maombi yetu ni kwamba mpate kuwa wakamilifu.
Hii ndiyo sababu nawaandikia mambo haya wakati sipo, ili nikija nisiwe mkali katika kutumia mamlaka yangu, mamlaka Bwana aliyonipa ya kuwajenga ninyi wala si ya kuwabomoa.
Hatimaye, ndugu zangu, kwaherini. Kuweni wakamilifu, mkafarijike, kuweni wa nia moja, kaeni kwa amani. Naye Mungu wa upendo na amani atakuwa pamoja nanyi.