Ninawaonea wivu, wivu wa Kimungu, kwa kuwa mimi niliwaposea mume mmoja, ili niwalete kwa Kristo kama mabikira safi.
Lakini nina hofu kuwa, kama vile Eva alivyodanganywa kwa ujanja wa yule nyoka, mawazo yenu yasije yakapotoshwa, mkauacha unyofu na usafi wa upendo wenu kwa Kristo.
Kwa sababu kama mtu akija na kuwahubiria Yesu mwingine ambaye si yule tuliyemhubiri, au kama mkipokea roho mwingine ambaye si yule mliyempokea, au Injili tofauti na ile mliyoikubali, ninyi mnaitii kwa urahisi.
Inawezekana mimi nikawa si mnenaji hodari, lakini ni hodari katika elimu. Jambo hili tumelifanya liwe dhahiri kwenu kwa njia zote.
Je, nilitenda dhambi kwa kujishusha ili kuwainua ninyi kwa kuwahubiria Injili ya Mungu pasipo malipo?
Nami nilipokuwa pamoja nanyi, nikipungukiwa na chochote, sikuwa mzigo kwa mtu yeyote, kwa maana ndugu waliotoka Makedonia walinipatia mahitaji yangu. Kwa hiyo nilijizuia kuwa mzigo kwenu kwa njia yoyote, nami nitaendelea kujizuia.
Kwa hakika kama vile kweli ya Kristo ilivyo ndani yangu, hakuna mtu yeyote katika Akaya nzima atakayenizuia kujivunia jambo hili.
Nami nitaendelea kufanya lile ninalofanya sasa ili nisiwape nafasi wale ambao wanatafuta nafasi ya kuhesabiwa kuwa sawa na sisi katika mambo wanayojisifia.
Watu kama hao ni mitume wa uongo, ni wafanyakazi wadanganyifu, wanaojigeuza waonekane kama mitume wa Kristo.
Kwa hiyo basi si ajabu, kama watumishi wa Shetani nao hujigeuza ili waonekane kama watumishi wa haki. Mwisho wao utakuwa sawa na matendo yao yanavyostahili.
Nasema tena, mtu yeyote asidhani kwamba mimi ni mjinga. Lakini hata kama mkinidhania hivyo, basi nipokeeni kama mjinga ili nipate kujisifu kidogo.
Ninayosema kuhusiana na huku kujisifu kwa kujiamini, sisemi kama vile ambavyo Bwana angesema, bali kama mjinga.
Kweli ni kwamba mnachukuliana na mtu akiwatia utumwani au akiwatumia kwa ajili ya kupata faida au akiwanyangʼanya au akijitukuza mwenyewe au akiwadanganya.
Kwa aibu inanipasa niseme kwamba sisi tulikuwa dhaifu sana kwa jambo hilo! Lakini chochote ambacho mtu mwingine yeyote angethubutu kujisifia, nanena kama mjinga, nami nathubutu kujisifu juu ya hilo.
Je, wao ni Waebrania? Mimi pia ni Mwebrania. Je, wao ni Waisraeli? Mimi pia ni Mwisraeli. Je, wao ni wazao wa Abrahamu? Mimi pia ni mzao wa Abrahamu.
Je, wao ni watumishi wa Kristo? (Nanena kiwazimu.) Mimi ni zaidi yao. Nimefanya kazi kwa bidii kuwaliko wao, nimefungwa gerezani mara kwa mara, nimechapwa mijeledi sana, na nimekabiliwa na mauti mara nyingi.
Mara tatu nilichapwa kwa fimbo, mara moja nilipigwa kwa mawe, mara tatu nimevunjikiwa na meli, nimekaa kilindini usiku kucha na mchana kutwa,
katika safari za mara kwa mara. Nimekabiliwa na hatari za kwenye mito, hatari za wanyangʼanyi, hatari kutoka kwa watu wangu mwenyewe, hatari kutoka kwa watu wa Mataifa; hatari mijini, hatari nyikani, hatari baharini; na hatari kutoka kwa ndugu wa uongo.
Nimekuwa katika kazi ngumu na taabu, katika kukesha mara nyingi; ninajua kukaa njaa na kuona kiu; nimefunga kula chakula mara nyingi; nimehisi baridi na kuwa uchi.