Tukamtuma Timotheo ambaye ni ndugu yetu na mtumishi mwenzetu wa Mungu katika kuieneza Injili ya Kristo, aje kuwaimarisha na kuwatia moyo katika imani yenu,
Kwa kweli, tulipokuwa pamoja nanyi tuliwaambia mara kwa mara kwamba tutateswa na imekuwa hivyo kama mjuavyo.
Kwa sababu hii nilipokuwa siwezi kuvumilia zaidi, nilimtuma mtu ili nipate habari za imani yenu. Niliogopa kwamba kwa njia fulani yule mjaribu asiwe amewajaribu, nasi tukawa tumejitaabisha bure.
Lakini sasa Timotheo ndiyo tu amerejea kwetu kutoka kwenu na ameleta habari njema kuhusu imani yenu na upendo wenu. Ametuambia kwamba siku zote mnatukumbuka kwa wema na kwamba mna shauku ya kutuona kama vile sisi tulivyo na shauku ya kuwaona ninyi.
Je, tutawezaje kumshukuru Mungu kiasi cha kutosha kwa ajili yenu, kutokana na furaha tuliyo nayo mbele za Mungu wetu kwa sababu yenu?
Usiku na mchana tunaomba kwa bidii ili tupate kuwaona tena na kujaza kile kilichopungua katika imani yenu.
Bwana na auongeze upendo wenu na kuuzidisha kati yenu na kwa wengine wote, kama vile tulivyo na upendo mwingi kwenu.