Napenda mfahamu kwamba kichwa cha kila mwanaume ni Kristo, na kichwa cha mwanamke ni mwanaume, nacho kichwa cha Kristo ni Mungu.
Naye kila mwanamke anayeomba au kutoa unabii pasipo kufunika kichwa chake, anakiaibisha kichwa chake, kwani ni sawa na yeye aliyenyoa nywele.
Kama mwanamke hatajifunika kichwa chake, basi inampasa kunyoa nywele zake. Lakini kama ni aibu kwa mwanamke kukata au kunyoa nywele zake, basi afunike kichwa chake.
Haimpasi mwanaume kufunika kichwa chake kwa kuwa yeye ni mfano wa Mungu na utukufu wa Mungu, lakini mwanamke ni utukufu wa mwanaume.
Kama vile mwanamke alivyoumbwa kutoka kwa mwanaume, vivyo hivyo mwanaume huzaliwa na mwanamke. Lakini vitu vyote vyatoka kwa Mungu.
Lakini mwanamke akiwa na nywele ndefu ni utukufu kwake? Kwa maana mwanamke amepewa nywele ndefu ili kumfunika.
Kama mtu anataka kubishana juu ya jambo hili, sisi wala makanisa ya Mungu hatutambui desturi nyingine.
Basi katika maagizo yafuatayo, siwezi kuwasifu, kwa sababu mkutanikapo si kwa ajili ya faida bali kwa hasara.
Kwanza, mnapokutana kama kanisa, nasikia kwamba kuna mgawanyiko miongoni mwenu, nami kwa kiasi fulani nasadiki kuwa ndivyo ilivyo.
kwa kuwa mnapokula, kila mmoja wenu anakula bila kuwangoja wengine. Mmoja hukaa njaa na mwingine analewa.
Je, hamna nyumbani kwenu ambako mnaweza kula na kunywa? Au mnalidharau kanisa la Mungu na kuwadhalilisha wale wasio na kitu? Niwaambie nini? Je, niwasifu juu ya jambo hili? La, hasha!
Kwa maana mimi nilipokea kutoka kwa Bwana yale niliyowapa ninyi, kwamba Bwana Yesu, usiku ule aliposalitiwa, alitwaa mkate,
naye akiisha kushukuru, akaumega, akasema, “Huu ndio mwili wangu, uliotolewa kwa ajili yenu. Fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu.”
Vivyo hivyo baada ya kula, akakitwaa kikombe, akisema, “Kikombe hiki ni agano jipya katika damu yangu. Fanyeni hivi kila mnywapo, kwa ukumbusho wangu.”
Kwa hiyo, mtu yeyote alaye mkate huo au kukinywea kikombe hicho cha Bwana isivyostahili, atakuwa na hatia ya dhambi juu ya mwili na damu ya Bwana.
Kwa maana mtu yeyote alaye na kunywa pasipo kuutambua mwili wa Bwana, hula na kunywa hukumu juu yake mwenyewe.